SIKUKUU YA EID AL FITRI MADEREVA WAPEWA ONYO, WAZAZI WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO.

 


Kuelekea sikukuu ya Eid al Fitr Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mnadhimu wa Jeshi la Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wilbert Siwa Aprili 09, 2024 katika mahojiano ya moja kwa moja kupitia kipindi cha redio - Dream fm 91.3 ya Jijini Mbeya.

Afisa Mnadhimu Siwa amewataka madereva kuacha matumizi ya vileo na kuendesha chombo cha moto kwani ni hatari kwa usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

"Ni wito wa Jeshi la Polisi kwa madereva wote kuepuka kutumia kilevi na kutaka kuendesha gari, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, hivyo likimbaini dereva aliyetumia kilevi, litamkamata, litampima kiwango cha ulevi na kumchukulia hatua za kisheria ikiwemo kumfikisha mahakamani na kumfungia leseni yake" alisema Afisa Mnadhimu Siwa.

Naye, Msaidizi wa Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mbeya, Mkaguzi wa Polisi Lovenes Mtemi amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto huku alisisitiza suala la ulinzi na usalama wa mtoto.

"Wazazi na walezi, kumbukeni kuwa jukumu la usalama wa mtoto ni lenu, usimuache mtoto wako bila muangalizi, usiache mtoto akaenda mwenyewe matembezi bila mtu mzima wa kumuangalia kwani ni hatari kwa usalama wake" alisisitiza Mkaguzi wa Polisi Mtemi.

Wakati huo huo, Msaidizi wa Polisi Jamii Mkoa, Mkaguzi wa Polisi Frida Mng'anya amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Mbeya kutoa ushirikiano kwa Wakaguzi wa Kata na Polisi Kata waliopo katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi kufanya doria katika mitaa ili kuzuia uhalifu.

Kuelekea sikukuu ya Eid al Fitr, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri na kuwahakikisha ulinzi na usalama wakazi wa Mkoa huo pamoja na wageni watakaoingia kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments