Aliyekuwa nahodha wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba yupo katika wodi ya wagonjwa mahututi huko Zambia baada ya kupata ajali ya gari iliyotokea katikati ya Kafwe na Lusaka, Zambia, leo.
Kalaba, 37, amepata ajali hiyo baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwamo ikiendeshwa na mwanamke ambaye hajafahamika kugongana uso kwa uso na lori la mafuta.
Awali, staa huyu aliripotiwa kuwa amefariki kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TP Mazembe katika ukurasa wao wa mtandao wa Facebook kabla ya baadaye miamba hao wa Afrika kutoa taarifa nyingine iliyoeleza kwamba gwiji wao huyo hajafa bali yupo kwenye hali mbaya.
Kwa mujibu wa Polisi wa Zambia, “uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ajali ilitokea baada ya gari aina ya Benz kujaribu kuipita gari nyingine bila ya tahadhari, na kusababisha kwenda kulivamia lori lililokuwa linakuja.”
Kabla ya kustaafu soka Julai mwaka jana akiwa na Mazembe, Kalaba alikuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa timu hiyo akiisaidia kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015 ambalo nyota mwenzake wa wakati huo Mbwana Samatta alimaliza mfungaji bora wa michuano hiyo na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza soka ndani ya bara hili.
0 Comments