Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM
nchini Tanzania imemteua Dkt. Bashiru Ali Kakurwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama
hicho.
Aidha Raymond Mangwala ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Vijana (UVCCM) ndani ya chama hicho tawala katika mkutano wa siku mbili uliomalizika
jijini Dar es Salaam.
Siku ya Jumatatu CCM kilipokea barua ya kustaafu ya aliyekuwa
Katibu Mkuu wa chama hicho tawala Abdulrahman Kinana.
Akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa chama cha CCM rais
wa Tanzania John Magufuli amepongeza kazi iliyotokana na tume iliyokuwa chini
ya uongozi wa Dkt Bashiru iliyoshughulika na uhakiki wa mali za chama na kusema
kwamba anatumai kuwa katibu mkuu huyo mpya atatumia aliyoyaona katika
kukiendeleza chama katika wadhifa huo mpya.
'Tumekupa jukumu hili tukiwa na matumaini makubwa kwamba yote
uliyoyaona kwa miezi mitano sasa ukayafanyie kazi katika Chama chote na jumuia
zake kwa nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM', amesema Rais Magufuli.
Kuondoka kwa Kinana ndani ya Chama kulizua maswali kuhusiana na
nani ataweza kuvaa viatu vyake, na hasa baada ya kurejea kazi alizozifanya za
kisiasa kwani Kinana aliongoza kampeni za rais wa awamu ya tatu Benjamini
Mkapa, na kusimamia kazi mbali mbali za utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Falsafa yake ya kijamaa, imejenga wasifu wa nje wa Kinana
unaoakisi kusimamia kile alichokiamini ndani ya chama chake,huku akitajwa
kubobea katika uenezi na ambaye amepata mafunzo katika nchi mbali mbali za
kikomunisti jambo ambalo linazidisha kuendelea kuhitajika kwake hata alipoamua
kustaafu.
Hata hivyo katika shughuli za ujenzi wa chama akiwa katibu mkuu
wa chama , Kinana alizunguka nchi nzima kufanya shughuli mbali mbali za chama
akishirikiana na watu katika kazi za mikono na kula nao chakula jambo ambalo
linatajwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa kwamba lilikiimarisha
zaidi chama hicho na kuongeza mshikamano.
Ni mtu ambaye amekuwa akiiamini na kuitekeleza falsafa ya
kijamaa,haiba yake ikionyesha uwezo wa kujenga umoja na kuunganisha watu ndani
ya chama chake,kuondoka kwake kuna acha swali kwamba je ni nani baada yake
atakayevaa viatu vyake,hilo ni jambo la kusubiria moshi mweupe kutoka ndani ya
kikao cha halmashauri kuu ya chama taifa ambacho kimeendelea kwa siku ya mbili .
Abdulrahman Kinana alizaliwa miaka 66 iliyopita Arusha, Kaskazini mwa Tanzania
Kinana ni mwanasiasa nguli aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Alihitimu shahada
yake katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani akibobea kwenye masuala ya
mikakati
Alikuwa
Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga taifa naibu Waziri wa mambo ya nje na
uhusiano wa kimatafa na Waziri wa ulinzi.
Kinana
aliwahi kufanya kazi na Jeshi la wananchi la Tanzania kwa miaka 20 kabla ya
kusaafu akiwa na cheo cha ukanali mwaka 1972.
Abdulrahman
Kinana pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika mashariki mwaka 2001 mpaka
mwaka 2006.
Ni mwanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alikuwa mstari wa
mbele katika kampeni za urais kuanzia mwaka 1995 wakati Rais Benjamini Mkapa
alipokuwa katika harakati za kuwania urais halikadhalika katika kipindi cha
Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kinana aliwahi kuwa mwakilishi wa diplomasia wa rais wa Tanzania
katika eneo la maziwa makuu na kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa mawaziri wa
ulinzi wa nchi za kusini mwa Afrika, SADC wakati huo akiwa Waziri wa ulinzi
katika serikali ya Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
0 Comments