Katika kuleta tija juu ya zoezi la chanjo ya awamu hiii ya pili wataalamu wa wizara ya afya mkoa wa Singida,wameshauriwa kutumia watu waliochanjwa dhidi ya Corona kutoa ushuhuda kwamba chanjo hiyo haina madhara ya aina yo yote,na kwa njia hiyo kasi ya uchanjaji itaongezeka kwa kiwango cha kuridhisha.
Wito huo umetolewa juzi na baadhi ya waandishi wa habari mkoani hapa,waliohudhuria semina ya siku moja.Semina hiyo ilihusu kuwaelimisha waandishi hao juu ya ugonjwa Corona, ili waweze kutambua wajibu wao wa kutoa taarifa sahihi kwa jamii.Ili iweze kupata chanjo hiyo muhimu kwa kinga ya mwili.
Wamesema kwa vile maneno mengi yamesemwa ya upotoshaji dhidi ya chanjo ya Corona,kasi ya uchajaji imekuwa ndogo mno.
“Upotoshaji huo umewaogofya wananchi wengi ambao wamepata hofu kupata chanjo.Hivyo nguvu zaidi zinahitajika katika kuwabadilisha wananchi waweze kujua umuhimu wa chanjo.Nguvu hiyo itaongezwa na sisi waandishi wa habari, pamoja na watu waliokwisha kupata chanjo ya Corona”,amesema mwandishi habari huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kwa upande wake mmoja wa wawesheshaji wa semina hiyo,Dk.Abdalah Balla,amefafanua kwamba chanjo ya Corona inawezesha kinga mwilini kupambana na virusi vya Corona, pale mtu anapoambukizwa.
Aidha,ametaja faida za chanjo kuwa ni kupambana na ugonjwa kwa kuzuia maambukizi,kupunguza hatari au makali ya ugonjwa hata kama mtu ameambukizwa na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Corona.
Kuhusu usalama wa chanjo hiyo,amesema chanjo hiyo ni salama kwa vile imejaribiwa kupitia tafiti mbalimbali za kisayansi na imethibitishwa na shirika la afya duniani.Na imethibitishwa na wizara ya afya kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA).
Dk.Balla ambaye pia ni mratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi mkoani hapa,ametumia fursa hiyo kuwahimiza waandishi wa habari kutumia kalama zao vizuri, kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kukinga miili yao dhahi ya Corona,kwa kupata chanjo.
Naye mjumbe wa kamati ya afya mkoa (PHC) na afisa maendeleo ya jamii,Patric Kasango,amesema kalamu za waandishi wa habari wa mkoa wa Singida,endapo zitatumika vizuri,zitachochea wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea,kupata chanjo dhidi ya Corona.
“Vyombo vya habari vinatumika kutoa taarifa sahihi mbalimbali zinazohusu mwenendo wa ugonjwa. Pia maelekezo muhimu yanayotolewa na serikali na wataalamu wa afya, kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huu ambao ni tishio kwa sasa”,amesema.
0 Comments